Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, mkusanyiko mkubwa na wa kifahari wa “Shahidi wa Umma” ulifanyika katika uwanja wa kihistoria wa Minar-e-Pakistan mjini Lahore kwa lengo la kuienzi hadhi ya juu ya kiongozi shahidi wa Umma wa Kiislamu, Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Khamenei, na kusisitiza kuiunga mkono Iran pamoja na kuimarisha mwamko na mshikamano wa Umma wa Kiislamu.
Mkusanyiko huo mkubwa, ambao umetajwa kuwa miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya wananchi katika miaka ya hivi karibuni, ulihudhuriwa na shakhsia mashuhuri za kidini, kisiasa, kijamii na kitamaduni kutoka sehemu mbalimbali za Pakistan. Aidha, mamia ya maelfu ya wananchi kutoka makundi mbalimbali ya jamii, wakiwemo wanaume, wanawake na watoto, walihudhuria kwa hamasa kubwa na kuonesha mfano wa mshikamano, mwamko na uaminifu kwa malengo na maadili ya Umma wa Kiislamu.
Katika hafla hiyo, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Jawad Naqvi, Mkuu wa Harakati ya Mwamko wa Umma wa Mustafa nchini Pakistan, alisema katika hotuba yake: “Kuandaliwa kwa mkusanyiko huu mkubwa ni alama ya mwamko wa fikra, mshikamano wa kitaifa na kuinuka kiwango cha ufahamu wa pamoja wa kijamii. Pia kunaonesha kwamba taifa la Pakistan linajiona kuwa sehemu ya harakati ya kimataifa ya kutetea haki na kuwaunga mkono wanaodhulumiwa.”
Aliongeza kuwa: “Mkusanyiko huu kwa hakika ni heshima kwa wote waliosimama upande wa haki, uadilifu na kuwatetea wanyonge, pia unatuma ujumbe wa wazi kwa dunia kwamba taifa la Pakistan halitanyamaza mbele ya dhulma, ukosefu wa haki na uchokozi.”
Mkuu wa Harakati ya Mwamko wa Umma wa Mustafa nchini Pakistan, akizungumzia sifa za madrasah ya kiongozi huyo shahidi, alisema: “Madrasah yake si nadharia tu au mkusanyiko wa mafundisho ya kifikra, bali ni njia ya vitendo na ya kujenga ustaarabu ambayo imejengwa juu ya msingi wa ‘kuwepo uwanjani’. Popote ambapo kutetea haki, kusimama dhidi ya dhulma, kuhudumia wananchi na kulinda maadili ya kibinadamu kunapokuwa ni jambo la lazima, Umma wa Kiislamu unapaswa kuwepo kwa namna ya kuwajibika na kwa ushiriki wa vitendo.”
Aliendelea kusema “Kiongozi shahidi, katika maisha yake yote yenye baraka na hata kupitia shahada yake, aliufikishia Umma wa Kiislamu ujumbe kwamba kuwajibika, kuwepo kwa ufanisi katika medani mbalimbali na kusimama imara mbele ya mabavu ni miongoni mwa masharti ya uhai na heshima ya Umma. Aliweza kupitia mwenendo wake, fikra zake na jihadi zake kufufua roho ya matumaini, muqawama na kujiamini miongoni mwa mataifa, na kuwahamasisha kurejea katika ushiriki wa vitendo katika nyanja mbalimbali za maisha.”

Maoni yako